UCHAMBUZI WA FASIHI SIMULIZI
TAKADINI
FANI:
MWANDISHI: BEN J. HANSON
WACHAPISHAJI: MATHEWS BOOKSTORE AND STATIONARIES
MWAKA: 2004
JINA LA KITABU
Jina la kitabu TAKADINI lina maana ya “Sisi tumefanya nini”. Hili ni jina ambalo Sekai alimpa mwanae mara baada ya kumzaa. Jina hili lilitokana na majonzi aliyokuwa nayo juu ya kutaka kuuawa kwa mwanae na yeye ilihali hawakuwa na hatia, ila tu kwa sababu ya mila za jamii yake zilivyotaka. Jina hili la kitabu ni sadifu kwani linasawiri vyema maudhui yaliyomo katika kitabu hiki. “Sisi tumefanya nini?’ ni swali ambalo linatokana na ukosefu wa haki ya kuishi, kubaguliwa kutopendwa, na hata kutengwa kwa watu wenye matatizo katika jamii. Swali hili linawalelekea wanajamii ambao bado wanashikilia mila potofu zinazowakandamiza na kuwanyanyasa watu wenye matatizo mfano, ulemavu wa ngozi, wagonjwa nk. Jina hili pia ni sadifu kwa maisha ya jamii yetu ya watanzania kwani watu bado wanashikilia mila potofu ambazo si nzuri. Mwandishi ametumia jina hili makusudi ili kutaka kuionesha jamii hali halisi ya vilio vya albino, wasichana wadogo wanaolazimishwa kuolewa nk. Kuwa huu sasa ni muda mwafaka wa jamii kuyaacha na kutupilia mbali mambo hayo.
MUUNDO
Muundo alioutumia mwandishi wa riwaya hii ni muundo wa msago au kwa jina lingine muundo wa moja kwa moja. Ameyapanga matukio katika mtiririko sahili kwani ameanza kutuonesha toka mwanzo mpaka mwisho wa maisha ya kijana Takadini “Msope”.Toka kutungwa kwa mimba yake, kuzaliwa kwake na kuishi kwake, matatizo na changamoto zinazomkumba na jinsi anavyokabiliana nazo na hatma ya maisha yake.
Mgawanyo wa visa na mtukio umepangwa katika sura ambapo visa vimejengwa kwa ufundi na kuvifanya vijengane na kukamilishana kuelekea kilele cha masimulizi. Matukio haya yamewekwa katika sura kumi na tatu.
Sura ya Kwanza
Sura hii inaanza kutuelezea kuhusu mwanamke Sekai anavotunga mimba, pia tunaelezwa kuhusu mtazamo mbaya wa wake wenzie juu ya mimba hiyo baada ya Sekai kukaa kwa muda mrefu bila ya kujaliwa mtoto.
Sura ya Pili
Hapa tunasimuliwa jinsi Sekai anavyofanikiwa kujifungua salama. Lakini kwa bahati mbaya kwa kawaida ya jamii yao anajifungua mtoto Zeruzeru ambaye kwa mila zao mtoto huyo ni laana. Hivyo alipaswa kutupwa mara moja ama kuuawa. Hakuna ambaye alikuwa tayari kumpokea mtoto yule kwani si baba yake wala jamii yake ila mama yake pekee.
Sura ya Tatu
Jamii bado haipo tayari kumpokea mtoto Sope, wanawake wenza wa Sekai wanasubiri kwa hamu kuona tukio la kutupwa kwa Takadini litakavokuwa, kwani ndio jinsi mila na taratibu za mababu zilivyotaka. Kutokana na hali hii ndipo Sekai anapata wazo la kutoroka. Anaamua kuondoka kwenda mbali ili kukinusuru kichanga kisicho na hatia kwani alisubiri kwa hamu na uchu wa muda mrefu kupata mtoto.
Sura ya Nne
Sekai anafanikiwa kutoroka na mwanae Takadini ili kumuepusha na kifo, jamii na Mtemi wanapata habari ya kutoroka kwake. Upelelezi unafanyika lakini juhudi hazikuzaa matunda kumpata Sekai na mwanae mchanga waliotakiwa kuuawa. Sekai anasafiri mbali na kufikia kijiji kingine na kupokelewa na mzee Chivero.
Sura ya Tano
Sekai anapokelewa katika kijiji cha mzee Chivero, jamii na wazee wanashitushwa sana na ujio huo lakini wanalazimika kumpokea tu baada ya malumbano ya muda mrefu. Kwani mila ziliwataka kutowatelekeza wageni katika kijiji chao, na hiyo ndiyo inakuwa mwanzo wa matumaini ya Sekai kuhusu kuishi kwa mwanae ambaye alionekana kuwa ni laana ya mababu na hakupaswa kuishi.
Sura ya sita
Baada ya Sekai kupokelewa katika kijiji cha mtemi Masasa, habari za ujio wake zinaenea kwa wanakijiji wote na wanaonekana kushtushwa sana, si hivo tu bali pia wanajiapiza katu kutomsogelea Sope kwani waliamini amelaaniwa. Lakini kwa juhudi za mzee Chivero baba mpya mlezi wa Takadini Sekai anapata rafiki. Tendai mke wa mtemi Masasa. Anajengewa kibanda cha kuishi yeye na mwanae na maisha yanaanza.
Sura ya saba
Sekai anaanza kujishughulisha na shughuli za kawaida kama mama na mwanamke, analima bustani na kufanya kazi ndogo za nyumbani. Siku moja katika safari ya kurudi nyumbani kwa bahati mbaya wanavamiwa na nyuki na kujeruhiwa vibaya yeye na mwanae, anaamua kumtupia mwanae kichakani ili kumuokoa na yeye kujitumbukiza mtoni. Wote wawili wanafanikiwa kutibiwa na kupona majeraha.
Sura ya nane
Taratibu Takadini anaanza kukua lakini anagundulika kuwa hawezi kutembea vyema kwa mguu mmoja, hii ilitokana na kuvunjika Mguu baada ya kurushwa kichakani na mamaye kama juhudi za kumwokoa. Hali hii inamhuzunisha zaidi Sekai na Chivero kwani walimpenda sana. Hapa ndipo mapenzi ya Chivero yalianza kudhihirika rasmi kwa Takadini kwani alijenga urafiki naye na kumpenda kama mwanae. Alimfundisha utabibu wa dawa za kienyeji na mambo mengine mengi. Pia tunaona watoto jinsi walivyombagua Takadini kutokana na hali yake, kwani waliambiwa na wazazi wao wasicheze naye amelaaniwa hivo hawakuthubutu.
Sura ya tisa
Katika sura hii, Mzee Masasi anafariki dunia na kumuacha mzee Chivero katika majonzi makuu. Hali ya mzee Chivero nayo inaanza kuzorota kwa uzee. Anampa Takadini usia mbalimbali na kumfunza. Pia tunaelezwa juu ya fikra mpya za Takadini za kupiga “mbira” kifaa cha muziki cha kijadi, hii baada ya kuvutiwa na sanaa hiyo aliposhiriki sherehe za mavuno za mwaka. Jamii bado ilimtenga Takadini na kumbagua, walimwona si binadamu bali mzuka tu! Na kwa bahati mbaya mzee Chivero naye aliaga dunia na kuacha simanzi kuu kwa Sekai na Takadini mbao alikuwa ni tegemeo na faraja kwao.
Sura ya kumi
Baada ya kifo cha mzee Chivero, Takadini anapata mwalimu maarufu mpiga mbira mzee Kutukwa, anamfundisha kupiga mbira, Takadini anaonesha juhudi kuu na kufanikiwa. Pia anmsaidia kifaa cha kumsaidia kutembea kutokana na mguu wake mbovu, hii inakuwa ni faraja kubwa kwa Takadini na mamaye
.
.
Sura ya kumi na moja.
Hapa tunaelezwa juu ya kijana Nhamo adui mkuu wa Takadini kwani hakumpenda na alimdhihaki na kumdhalilisha mara kwa mara. Kijana huyu anaonekana kuwa ni shujaa katika jamii yake kwa kitendo cha kumuua simba mla mifugo. Hiyo inamletea sifa kubwa na majivuno mengi hivo wasichana wengi kumtamani awaoe, hali ni tofauti kwa Shingai ambaye anaonesha hisia za mapenzi kwa Takadini pamoja na hali yake ya “Usope”. Chemchemi za mapenzi ya Takadini kwa Sekai zinaanza kumea jambo ambalo linamkera sana Nhamo na kuzidisha chuki kwa Takadini kwani pia alitamani kuwa na Shengai binti mrembo. Jamii inafanya kikao kujadili suala la Shengai kumpenda Takadini na wanalipinga vikali suala hilo.
Sura ya kumi na mbili
Nhamo anakata shauri na kwenda kumposa Shengai, wazazi wa pande zote mbili wanaliunga suala hilo mkono asilimia zote. Kwani hilo lingewanusuru aibu ya mwanao kuolewa na Sope, kwani walijua fika Shingai alimpenda Takadini na hakumtaka Nhoma. Nhoma anamuonya vikali Takadini kuwa asiendelee na lolote kwa Shengai. Pia hapa zinafanyika sherehe ya kijadi ya kumkaribisha hayati mzee Chivero tena nyumbani.
Sura ya kumi na Tatu
Wakati wa sherehe ya mavuno, binti Shengai anashindwa kuvumilia na kuamua kumfuata Takadini kibandani kwake. Anaamua kuvunja mila za kwao kwani alimpenda kwa dhati Takadini, pamoja na dharau, kejeli, kubaguliwa, ulemavu wake na kuonekana kuwa ni mtu aliyelaaniwa. Wazazi wake wanamtenga na kutomtambua kama ni mtoto wao tena. Suala hilo linatikisa jamii ya watu wa kijiji kile na hata kutaka kuwafukuza Sekai na mwanae lakini wanaokolewa na maamuzi ya busara ya wazee kwa kuwacha Shengai na mpenziwe Takadini waishi hali wakisubiri matokeo! Kuwa je mtoto atazaliwa sope? Na kuongeza ukoo wa masope na kijiji chao kuwa cha masope? Hapa ndio inapojulikana hatma ya Takadini na mkewe kwani anapata ujauzito na kufanikiwa kujifungua mtoto salama asiye Sope. Ilikuwa furaha kuu kwa mama na mtoto na wote pia. Wanaamua kurudi kijijini kwao walikotoroka ili kwenda kuwadhihirishia kuwa hata sope anaweza kuishi hapaswi kubaguliwa na kutengwa.
MTINDO
Mwandishi ametumia mitindo kadha wa kadha ili kuipamba kazi yake na kuifanya ivutie wasomaji; mfano matumizi ya nafsi mbalimbali, matumizi ya nyimbo nk.
Matumizi ya nafsi
Kwa kiasi kikubwa yametawala matumizi ya nafsi ya tatu umoja na wingi katika sura zote. Mfano.uk. 30. “ aliingia ndani na kuanza kazi.” Pia uk.3 “ Sekai alikoka moto nje ya kibanda, akaketi na kuzungumza na Pindai”.
- Matumizi ya nafsi ya pili au dayalojia
Mfano uk 29 - 30. Mazungumzo kati ya Chivero na Sekai
“je umelala salama?
Sijambo mwanangu, sijui wewe?
Sijambo Sekuru,
Na mwanao je?
Naye hajambo.”
- Matumizi ya nafsi ya kwanza. Mfano uk. 82 na 83
“lakini ghafla nilipata nguvu mpya”
“nilikuwa na nguvu kama kijana….”.
Pia mwandishi ametumia nyimbo katika baadhi ya sura ili kuwaburudisha na kuliwaza wasomaji. Mfano uk. 2 wimbo aliouimba mke mwenza wa Sekai Rumbdzai.
“Mashamba yetu yamelimwa
mbegu nazo zimepandwa
zimechipua na kumea,
sisi watatu tumepanda mavuno yetu;
mheshimiwa wetu amemiliki mavuno
kwa mikono yake halisi
kutoka mashamba yetu yote
lakini ni kipi alichoambulia
kutoka ardhi ile isiyomea kitu?”pia ametumia wimbo uk. 34, 57, 85.
mbegu nazo zimepandwa
zimechipua na kumea,
sisi watatu tumepanda mavuno yetu;
mheshimiwa wetu amemiliki mavuno
kwa mikono yake halisi
kutoka mashamba yetu yote
lakini ni kipi alichoambulia
kutoka ardhi ile isiyomea kitu?”pia ametumia wimbo uk. 34, 57, 85.
Matumizi ya hadithi ndani ya hadithi pia ni mtindo mwingine wa usimulizi alioutumia mwandishi. Mfano uk 82Kutukwa alisimulia vijana hadithi enzi ya ujana wake na jinsi alivopambana na maadui vitani.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi inayoeleweka kwa wasomaji wake. Ametumia pia lugha nyinginezo kama vile lugha za kikabila.Maneno kama vile “Amai”,lenye maana ya mama, “Sope” lenye maana ya zeruzeru, “shumba”- simba, “mbira” – chombo cha asili cha muziki, “gudza” – blanketi lililotengenezwa kwa nyuzi za magome ya miti. nk. Hivyo mwandishi ametumia lugha hii ili kuwaleta wasomaji kwenye mazingira halisi ya kiutamaduni ya jamii ile.
- Matumizi ya tamathali za Semi
Tashibiha
Mfano uk. 6 “ muda huenda polepole mithili ya mwendo wa kakakuona Uk.15 “ habari njema huchechemea kwa mguu mmoja lakina mbaya hukimbia kama Sungura”
Uk.16 “….. alibaki kama kinyago cha mpingo”.
Uk.28 “ sio kufurika kama Chura”
Uk.33 “aligeuza shingo yake sawa na Mbuni”
Uk.42 “ nywele kama vinyweleo vya mahindi yaliyokaribia kukomaa”
Uk.82 “muziki ulikuwa kama chemchemi ya maji mwilini mwake”
Tashihisi
Mfano uk. 5 “ndege mbalimbali wakiimba kuikaribisha siku mpya”
Uk. 7 “vivuli vya jioni viliongezeka urefu”
Uk. 18 “maneno yananila mifupa yangu”
Uk 25 “kifo kilinukia”
Tafsida
Mfano, uk. 83 “sehemu zake za siri”
Sitiari
Mfano, uk. 88 “ Tapfumaneyi aligeuka mbogo”
Uk.97 “mwana Mbwa hakuiba mfupa”, Tawanda mfupa ulikwenda wenyewe kucheza
naye.” Hapa mfupa umefananishwa na Shingai na Takadini ndio mwanambwa
Matumizi ya Semi
Methali
Uk. 45 “ kipofu huwa hachagui shimo la kutegea wanyama”
uk. 33 “ moyo mwema utakufanya uuwawe”
uk. 33 “ moyo mwema utakufanya uuwawe”
Misemo
Mfano. Uk. 12 “kufikiri katika siri ni sawa na safari ya mbwa”
Uk. 100 “kanga hawezi kutua juu ya bua la mtama”
Uk.101 “kibuyu kikubwa hakikosi mbegu ndani”
Uk. 125 “fuvu la nyanilimekuwa kijiko kwa mlo wa mahindi”
Nahau
uk. 27 “ penzi langu kwake halikufua dafu”
Uk. 88 “kutiana moyo wa ari”
- Matumizi ya mbinu nyingine za kisanaa
Nidaa
Mfano, Uk.4 “Ha!” , “Ha! Atimuliwe tena? Mchawi?”
Uk.16 “Mai, Wee!”
Uk.39. “Ha! Iwe! Ha!”
Mdokezo
Mfano Uk.3 “ndiyo Pindai, ninaogopa……….”
Uk.42 “mtu mzima kama watu wenine ameamua………”
Takriri
Mfano, uk 57 “ mwanangu, mwanangu, mwanangu, wamekufanya nini?”
WAHUSIKA
Sekai
- Ni mke wa Makwati wa kwanza.
- Ni mwanamke jasiri.
- Anapinga mila potofu na mbaya za jamii yake.
- Ni mvumilivu.
- Ni mchapakazi mzuri.
- Anajifungua mtoto zeruzeru ambaye ni laana kwa jamii yake.
- Ni mtiifu na mwenye adabu.
- Ana huruma na mnyenyekevu.
- Ana mapenzi ya dhati.
- Anafaaa kuigwa na jamii.
Takadini
- Ni mtoto anayezaliwa na ulemavu wa ngozi( albino)
- Anasadikika kuwa ni laana kwa jamii yake hivyo kupaswa kuuawa au kutupwa mbali.
- Anaokolewa na mama yake kwa kutoroshewa katika kijiji kingine.
- Anapokua anakua kijana jasiri.
- Hapendwi na jamii.
- Anabaguliwa na jamii, hana rafiki.
- Ni mvumilivu na msikivu mwenye heshima.
- Alimpenda Chivero sana.
- Alikuwa mpiga mbira (chombo cha muziki cha kijadi) maarufu.
- Alimuoa Shingai na kupata mtoto asiye Sope.
Makwati
- Mme wa Sekai.
- Ameoa ndoa ya mitara ana wake wanne.
- Anashikilia mila na desturi potofu.
- Hana mapenzi ya dhati kwa mwanae.
- Hafai kuigwa na jamii.
Dadirai na Rumbidzai
- Wake wengine wa mzee Makwati.
- Wana wivu.
- Hawampendi Sekai.
- Wana roho mbaya kwani wanamwombea Sekai mabaya.
- Ni katili kwani wanashinikiza Sekai na mwanae wauawe bila huruma.
- Wasengenyaji.
- Hawafai kuigwa na jamiii.
Pindai
- Mke wa pili wa Makwati.
- Ana upendo wa dhati kwa Sekai.
- Ni mkweli.
- Hana wivu.
- Ni mshauri mzuri.
- Anafaa kuigwa na jamii.
Chivero
- Ni mzee wa kijiji cha mzee Masasa.
- Anawapokea Sekai na mwanae baada ya kutoroka kwao kwa ukarimu mkubwa.
- Ni mwenye roho nzuri.
- Ana huruma sana.
- Ni mganga wa tiba za asili.
- Ana mapenzi ya dhati kwa Takadini na Sekai.
- Anamrithisha Takadini uganga.
- Ana busara na hekima.
- Ni mshauri mkuu wa Mtemi Masasa.
- Anafaa kuigwa na jamii.
Mtemi Masasa
- Ana busara na hekima.
- Ana huruma.
- Anafuata mila na desturi ya jamii yake.
- Ni msikivu.
- Ni rafiki mkubwa wa Chivero.
- Ni kiongozi bora.
Nhamo
- Ni kijana katika kijiji cha mtemi Masasa.
- Ana majivuno na jeuri.
- Hampendi Takadini kwani alimbagua kumpiga na hata kumdhalilisha.
- Hafai kuigwa n ajamii.
Tendai
- Mke mdogo wa mwisho wa mtemi Masasa.
- Aliolewa bila kupenda, hakumpenda mtemi Masasa kwani alimzidi umri.
- Alikuwa rafiki mzuri wa Sekai.
- Ana mapenzi ya dhati kwa Takadini.
- Ana bidii na mvumilivu.
Nhariswa na mkewe
- Ni wazazi wa Shingai
- Wanashikilia mila desturi potofu
- Hawakupenda kabisa kitendo cha mtoto wao kumpenda Takadini
- Walimlazimisha kuolewa na Nhamo kwani walitaka sifa na maujiko
- Walimtenga Shingai baada ya kutoroka na kuolewa na Takadini
- Si wazazi wazuri
- Hawafai kuigwa na jamii
Kutukwa
- Ni mzee katika kijiji cha mtemi Masasa
- Ni mpigaji mbira maarufu
- Alimfundisha Takadini kupiga mbira
- Alitoa mtazamo mbaya kwa wanakijiji wenzake kwa kuwaeleza sifa nzuri za Takadini
- Alimpenda Takadini. Anafaa kuigwa na jamii
MANDHARI
Mandhari aliyotumia Ben J Hanson ni mandhari ya kijijini kwani maisha ya watu na mazingira yanayoelezwa ni ya kijijini, masuala kama ya kilimo, ufugaji, sherehe za mavuno, makazi ya watu kukaa katika jumuiya ya pamoja kijamaa inayoongozwa na mtemi mmoja. Mfano mtemi Masasa, yote haya ni viashiria kuwa mandhari ni ya kijini. Mandahari ambayo mwandishi ameijengea mawazo yake na kuyaibua ni sadifu na halisi. Kwani maeneo ya vijijini ndiko kulikokithiri mambo ya imani potofu na za kishirikina kama vile kuwaua watoto Sope au albino.