JINA LA KITABU: NGOSWE PENZI KITOVU CHA UZEMBE
MWANDISHI: EDWIN SEMZABA
WACHAPISHAJI: NYAMBARI NYANGWINE PUBLISHERS
MWAKA: 2006
UTANGULIZI WA KITABU
Ngoswe penzi kitovu cha uzembe ni tamthiliya maarufu sana ambayo imewahi kuigizwa katika redio Tanzania na katika majukwaa mbalimbali hapa nchini. Ni tamthiliya ambayo imeundwa vyema katika vipengele vya fani na maudhui. Ameteua lugha nzuri na yenye mvuto kwa wasomaji yenye mbinu za kifasihi zilizosheheni, muundo wenye mtiririko mzuri, unaoakisi kuanza kuchipuka kwa matukio mpaka kilele cha matukio. Wahusika wamebeba vyema uhusika wao mfano Ngoswe.
Ameibua dhamira kuhusu mambo yanayoigusa jamii ya leo kama vile uzembe, madhara ya ulevi, uzembe kazini, suala la matabaka kati ya mjini na vijijini. Mtazamo, falsafa na msimamo wake ni kulenga kuibadilisha jamii na kuleta maendeleo.
JINA LA KITABU
Jina la kitabu “Ngoswe penzi kitovu cha uzembe” ni jina ambalo limesawiri vyema yaliyomo ndani ya kitabu hicho, kwani Ngoswe ndio jina la mhusika mkuu anayebeba dhamira kuu ya tamthiliya. Pia penzi limeonekana kuwa ni kitovu cha uzembe kwani ndio yaliyopelekea kuteketezwa kwa karatasi za takwimu za sensa. Hivyo jina la kitabu si tu kwamba limesawiri yaliyomo katika kitabu bali pia katika jamii.
FANI
MTINDO
Mtindo alioutumia mwandishi ni dayalojia au majibizano. Mwandishi amepanga visa na masimulizi kwa kutumia majibizano ya wahusika.
- Matumizi ya nafsi
Matumizi ya nafsi ya kwanza. Mwandishi ndiye ameyafafanua na kuelezea baadhi ya matukio. Katika karibu kurasa zote mwandishi ameonekana kuwa ndiye msimuliaji wa matukio.
Matumizi ya nafsi ya pili
Hapa watu wawili na zaidi wanajibizana. Tamthilya hii wahusika wanaojibizana kuibua dhamira na migogoro. Kuna majibizano baina ya mzee Mitomingi, Ngoswe na Mazoea nk.unaweza kupata mfano uk. wowote kwani ndio mtindo uliotawala.
MUUNDO
Muundo uliotumika ni muundo wa mojakwamoja au sahili. Kwani ameonesha tangu mwanzo wa mambo mpaka mwisho, anajenga visa vidogo mpaka visa vikuu au kileleni.
Amepanga visa na matukio yake katika maonesho matano. Kila kichwa kina maelezo yaliyojadiliwa katika onesho hilo.
KIJITO
Hapa yanaeleza jinsi mambo yanavyoanza. Jinsi Ngoswe anavyoingia kijijini anavyopokelewa na kuanza kufahamiana na wenyeji wake.
VIJITO
Hapa Ngoswe anaanza kufanya kazi iliyompeleka kijijini na tunaanza kuoneshwa changamoto anazokumbana nazo.
MTO
Ni mwendelezo wa matukio ya mwanzo hapa visa vinazidi kukua.
JITO
Hapa Ngoswe anakumbana na changamoto nyingi zaidi katika kazi yake. Na hapa anazidi kuanguka kwani anajiingiza katika mapenzi na msichana Mazoea, anaendekeza ulevi na kuharibu kazi kabisa.
BAHARINI
Hapa inaoneshwa mwisho wa mambo jinsi yalivyokuwa. Yanaonekana mahojiano baina ya Serikali na Ngoswe na Mitomingi juu ya uzembe uliofanyika wa kupoteza takwimu na hapa ndipo suluhisho linapotolewa juu ya matatizo hayo.
WAHUSIKA
NGOSWE
- Kijana wa kiume umri kati yamiaka 20-25
- Ameelimika na amestaarabika
- Anatumwa na serikali kufanya sensa kijijini
- Anajihusisha na mapenzi na msichana mazoea
- Ni mlevi
- Hana umakini katika kazi
- Aliharibu kazi ya serikali
- Hafai kuigwa na jamii
MAZOEA
- Ni msichana mwenye umri kati ya miaka 18-20
- Ni binti wa Mzee Ngengemkeni Mitomingi
- Hana elimu na hajastaarabika
- Ana nidhamu ya woga
- Ana tama
- Hana msimamo alikubali kuchukuliwa na Ngoswe hali akijua alishatolewa mahari
- Hafai kuigwa na jamii
NGENGEMKENI MITOMINGI.
- Ni balozi katika kijiji chake
- Ni baba mzazi wa Mazoea
- Ameoa ndoa ya mitara, ana wake wawili
- Hajaelimika
- Anashikilia mila na desturi za kale
- Mlevi
- Mkali sana
- Anateketeza karatasi za takwimu.
MZEE JIMBI
- Mwanakijiji
- Hajaelimika kwani hajui hata umri wake
- Ni mlevi
- Ana wake wawili
- Anashikilia ukale
MAMA MAZOEA
- Mke mkubwa wa Mitomingi
- Mama yake Mazoea
- Mlezi wa familia
- Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi katika familia
MAMA INDA
- Mke wa pili Mzee Mitomingi
- Mama yake Huzuni
- Hapewi nafasi ya kutoa maamuzi
- Ni mlezi wa familia.
MANDHARI
Mandhari ya tamthiliya hii imechorwa katika mazingira ya kijijini. Mambo yanayoelezwa ni ya kijijini mfano kilimo, hali ya watu kimaisha, huduma duni sana za kijamii kama vile shule, umbali wa makazi toka nyumba moja hadi nyingine. Haya yanatudhihirishia vyema mandhari hiyo ambayo kwayo imeibua dhamira mbalimbali kama vile umaskini, ukosefu wa elimu, huduma duni za afya vijijini, masuala ya imani potofu nk.
MATUMIZI YA LUGHA
Lugha aliyotumia mwandishi ni lugha fasaha na rahisi kueleweka kwa wasomaji. Pia kuna matumizi ya lugha nyingine mfano uk. 1 “bell bottom”
- Matumizi ya semi.
Methali
Uk.22 “Penye nia pana njia”.
Uk.27 “Waona vyaelea vyaundwa.”
Misemo
Uk.14 “Akuwaniae ujovu haji kweupe”
Nahau
Uk.11 “hebu keti tutupe mawe pangoni” – tule chakula
Uk.7 “mbongo zimelala”- ana maarifa
Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda”- anapenda pombe sana.
- Matumizi ya tamathali za semi.
Tafsida
Uk.21 “Wala hajarudi, kama ingekuwa ni kujisaidia si angekuwa amekwishamaliza?”
Tashbiha
Uk.1 “vumbi jekundu kama ugoro wa subiana”
Uk.8 “sarawili yake miguuni kama kengele ya bomani”
Uk.17 “wanaondoka huku wakitazamwa kama vile mizuka”
Sitiari
Uk.7 Mama Mazoea : “kiziwi mkubwa wee!”
Uk.14 “pombe na yeye ni pete na chanda!”
Uk.26. “karatasi? za takwimu? Ndio wanyama gani hao?”
Mubaalagha
Uk.11 Mama Mazoea : “kupeleka chakula ndio umefanya makao!”
Mama mazoea : “Kujibu swali ndio ukachukua mwaka mzima!”
- Mbinu nyingine za kisanaa
Mdokezo
Uk.22 Mazoea : “sijui….. siwezi….. namuogopa baba”
Uk.16 Ngoswe : “huyo mtoto wenu wa kwanza anaishi hapa au…..”
Takriri
Uk.9 “Mama Masikio! We Mama Masikio!”
Uk.13. “Hodi! Hodi!”
Uk.2 “karibu karibu”
Tashtiti
Uk.5 Ngoswe: “hivyo waitwa nani?”
Mazoea: “mie?”
Uk.22 Ngoswe: “mchumba? Kwani mchumba ni kitu gani?”
Uk.26 Mitomingi: “karatasi? Za takwimu? Ndio wanyama gani hao?
Hapa wahusika waliuliza maswali ambayo majibu yake waliyaelewa ila kutokana na kutaka kudhihirisha hasira, msisitizo nk. Ndio maana wametumia tashtiti.
Onomatopea/tanakali sauti
Uk.7 Kifaruhande anacheka “Ha! ha! ha!
- Ujenzi wa taswira
Mwandishi ametumia taswira ya mto kuelezea visa vyake. Sehemu ya kwanza ni sehemu ya kijito, kijito ni kimto kidigo mwandishi hapa anaanza kueleza mambo yakiwa machanga kabisa ndio yanaanza.
Sehemu ya pili ni vijito. Huu ni muunganiko wa vijito vidogovidogo hapa mwandishi anaanza kueleza visa vidogovidogo. Sehemu inayofuata ni sehemu ya Mto. Hii inaashiria mambo yameanza kuwa mazito, visa vinakua zaidi na Ngoswe anazidi kuingia katika changamoto kubwa zaidi.
Pia Jito ni taswira ambayo mwandishi ameitumia kuashiria hatari zaidi mambo makubwa zaidi na hapa ndipo tunaona Ngoswe anaanguka kabisa katika kazi yake kwani Jito ni lenye maji mengi na yanayoenda kwa kasi hivyo huhitaji umakini mkubwa zaidi.
Mwisho sehemu ya Bahari ambapo hapa ndipo hatima ya mambo inaelezwa Ngoswe anazama na kupotea kabisa! Hafanikiwi kutoa takwimu kwani karatasi zilichomwa moto.